Monday 16 April 2018

Watu 257 wafa kwenye ajali ya ndege Algeria

Watu 257 wafa kwenye ajali ya ndege Algeria

Takriban watu 257 waliokuwa kwenye ndege ya kijeshi nchini Algeria wamefariki dunia baada ya ndege hiyo kuanguka nje ya mji mkuu wa nchi hiyo Algiers. Ndege hiyo iliwaka moto baada ya kuanguka.
Militärflugzeug in Algerien abgestürzt (Reuters/R. Boudina)
Takriban watu 257 waliokuwa kwenye ndege ya kijeshi nchini Algeria wamefariki dunia baada ya ndege hiyo kuanguka nje ya mji mkuu wa nchi hiyo Algiers hii leo. Kulingana na shirika la habari la serikali, ndege hiyo iliwaka moto baada ya kuanguka katika tukio linalotajwa kuwa baya zaidi kwenye usafiri wa anga kuwahi kushuhudiwa nchini humo. 
Picha zilizorushwa na kituo kimoja cha televisheni kinaonyesha watu na magari ya msaada wa dharura wakiwa wamefurika kuzunguka eneo hilo la ajali lililotawaliwa na moshi na moto, karibu na uwanja wa ndege wa kijeshi kwenye kambi ya Boufarik kusinimagharibi mwa Algiers. 
Wizara ya ulinzi imesema, jumla ya watu 257 wamekufa, wengi miongoni mwao ni wanajeshi. Wahudumu 10 wa ndege na baadhi ya abiria waliokufa wamekwishatambuliwa na jamaa zao. Imeongeza kuwa manusura kadhaa wanaendelea kupata matibabu katika hospitali ya jeshi, na miili ya wahanga wa ajali hiyo imepelekwa hospitalini hapo kwa ajili ya utambuzi.
Chanzo cha ajali bado hakijajulikana na tayari kumeanzishwa uchunguzi.
Militärflugzeug in Algerien abgestürzt (Reuters/Ennahar Tv)
Ni tukio la kwanza kwa ndege za jeshi la algeria kutokea tangu mwaka 2014.
Mmoja wa wanachama wa chama tawala cha National Liberation Front, FLN, amekiambia kituo binafsi cha televisheni kwamba miongoni mwa waliokufa ni wanachama wa kikundi cha wanaotaka uhuru wa taifa jirani la Sahara Magharibi, la Polisario, linaloungwa mkono na serikali ya Algeria. Eneo hilo la Sahara Magharibi linazozaniwa kwa muda mrefu na Morocco na Algeria. 
Ni miongoni mwa matukio yaliyowahi kutokea, ingawa hili ni baya zaidi.
Ndege hiyo ilikuwa inaelekea katika mji wa Tindouf, ulioko mpakani mwa Algeria na Sahara Magharibi, lakini ilianguka katika eneo la uwanja wa ndege, hii ikiwa ni kulingana na wizara ya ulinzi. Tindouf ni makazi ya maelfu ya wakimbizi na wengi wakitokea Sahara Magharibi, ambao miongoni mwao ni wafuasi wa Polisario.  
Kulingana na kituo cha televisheni cha Dzair, watu watano wako katika hali mbaya. Mkulima mmoja amekiambia kituo cha televisheni cha Ennahar kwamba aliwaona baadhi ya abiria waliruka kutoka kwenye ndege hiyo kabla ya kuanguka. 
Ofisi ya waziri mkuu imesema wabunge walisimama kimya kwa dakika moja kuwaombea wahanga wa ajali hiyo. 
Ndege hiyo chapa 11-76 iliyoundwa nchini Urusi miaka ya 1970 kwa muda wote imekuwa na rekodi nzuri ya kiusalama. Imekuwa ikitumiwa kwa usafirishaji wa mizigo na abiria. 
Tukio hili ni la kwanza kwa ndege za jeshi la Algeria kutokea, tangu lile la mwezi Februari mwaka 2014, ambapo ndege iliyotengenezwa nchini Marekani chapa C-130 Hercules turboprop ilipoanguka kwenye milima ya Algeria, na kusababisha vifo vya watu 76 na mmoja tu alinusurika.
Tukio baya zaidi la ajali ya ndege kutokea kwenye ardhi ya Algeria ni la mwaka 2003, wakati watu 102 walipokufa na mmoja kunusurika baada ya ndege ya kiraia kuanguka ilipofika mwishoni mwa njia ya kurukia katika uwanja wa Tamanrasset. 

No comments: