Winnie Mandela apewa mazishi ya kitaifa
Maelfu ya watu wamekusanyika Jumamosi (14.04.2018) katika uwanja wa mpira wa Soweto kutoa heshima zao za mwisho kwa mwanaharakati wa kupinga ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini Winnie Madikizela-Mandela.
Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa ametoa heshima yake iliyojawa hisia akiahidi kupendekeza Bi. Winnie apokee heshima ya juu ndani ya chama tawala cha African National Congress ANC. Ramaphosa amemtaja Winnie kama mtu aliyekuwa akijivunia, mtetezi na mwenye kueleza kwa ufasaha aliyefichua uongo wa wabaguzi.
Amesema kuwekwa kizuizini, mateso na miaka ya marufuku ambayo Madikizela-Mandela alipitia, vilimtia hamasa kama mwanaharakati wa kisiasa, lakini pia vilisababisha majeraha makubwa ambayo hayajawahi kupona na kwa kiasi kikubwa kupuuzwa na rika nyingi.
Winnie Madikizela-Mandela aliyefariki Aprili 2, akiwa na umri wa miaka 81 amezikwa kwa heshima ya kitaifa ambapo jeneza lake lilibebwa na askari wakati mwili wake ukiingizwa katika uwanja wa Soweto.
Viongozi kadhaa wa nchi walihudhuria mazishi hayo akiwemo rais wa Congo Brazzaville Denis Sassou Nguesso, waziri mkuu wa taifa jirani la Lesotho Pakalitha Mosisili; na wajumbe wengine kutoka serikali za afrika na vyama vya ukombozi. Marais wa zamani wa Afrika Kusini Jacob Zuma na Thabo Mbeki pia nao walihudhuria mazishi ya mpambanaji huyo aliyejulikana mama wa taifa au mama Winnie.
Mwandishi: Radick Nap Africa
Mhariri: Rama Dee
No comments:
Post a Comment